Rukwa kufunguka kiuchumi, Tanzania kuuza umeme Mataifa ya jirani
MAKAMU wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Deogratius Ndejembi amesema kukamilika kwa mradi wa Kituo cha Kupoza na Kusambaza Umeme cha Malangali, mkoani Rukwa, kutafungua ukurasa mpya wa maendeleo ya kiuchumi kwa kuimarisha upatikanaji wa umeme wa uhakika, kuvutia wawekezaji na kuwezesha Tanzania kuuza umeme Mataifa Jirani.
Akizungumza wakati wa ziara yake ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa kituo hicho, Makamu wa Rais amesema Mkoa wa Rukwa wenye mahitaji ya takribani Megawati 30, kwa sasa unapokea Megawati 16 pekee, hali iliyokuwa ikikwamisha shughuli za uzalishaji, hususan uchakataji wa mazao ya kilimo na madini.
Amesema Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imewekeza katika mradi huo ili kuhakikisha Rukwa inaunganishwa na Gridi ya Taifa na kuwa kitovu cha uzalishaji na biashara ya umeme katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kusini mwa Afrika.
“Leo hii TANESCO inanunua umeme Zambia, lakini kwa laini hii sisi tutaanza kuiuzia Zambia umeme mkubwa na wa uhakika,” amesema Makamu wa Rais, huku akiwataka wawekezaji kuchangamkia fursa za kiuchumi mkoani Rukwa na wananchi kulinda miundombinu hiyo.
Awali, Naibu Waziri wa Nishati, Salome Makamba, amesema mradi huo ni sehemu ya uwekezaji wa Serikali unaodhihirisha dhamira ya dhati ya kuhakikisha mikoa yote nchini inaunganishwa na Gridi ya Taifa.
Amesema asilimia 90 ya wafanyakazi wanaotekeleza mradi huo ni Watanzania, huku akieleza kuwa majaribio ya mitambo yanatarajiwa kuanza katikati ya Novemba 2026.
Akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa mradi huo, Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Umeme nchini (TANESCO), Lazaro Twange, amesema ujenzi wa kituo cha Malangali umefikia asilimia 85.17, huku kazi za kuwasha na kuingiza umeme zikipangwa kukamilika Novemba 2026.
Amesema kituo hicho kinachojengwa na kampuni ya TBEA kutoka China kwa gharama ya Shilingi Bilioni 161.9, kitakuwa na uwezo wa kupokea umeme wa Kilovolti 400 na kuushusha katika misongo ya Kilovolti 220, 66 na 33, kikijumuisha transfoma nne na njia nane za kusambaza umeme katika maeneo mbalimbali ya Mkoa wa Rukwa.
Kukamilika kwa mradi huo kunatarajiwa kuondoa changamoto ya upungufu wa umeme, kuchochea ujenzi wa viwanda, kuongeza thamani ya mazao na kufungua fursa mpya za ajira na uwekezaji, huku Tanzania ikiimarisha nafasi yake katika biashara ya nishati kikanda.
The full article is being collected. Available text is shown for now.