DED KIBITI ATOA ONYO KWA WATUMISHI WANAOTOROSHA KOROSHO, ASEMA HATOVUMILIA

Na Mwamvua Mwinyi, Kibiti
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kibiti, Ramadhan Kimara, ameonya kuwa hatamvumilia mtumishi yeyote atakayehusika na utoroshaji wa korosho, akisisitiza kuwa vitendo hivyo vinahatarisha mapato ya halmashauri.
Kimara ametoa onyo hilo Oktoba 13, 2026, wakati akizungumza na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini cha halmashauri hiyo, baada ya kukamilika kwa Mkutano wa Wadau wa Tasnia ya Zao la Korosho wilayani humo.
Ameeleza korosho na ufuta ni miongoni mwa mazao yenye mchango muhimu katika kuongeza mapato ya ndani ya halmashauri, hivyo udhaifu katika usimamizi unaweza kusababisha mazao hayo kutoroshwa na kuikosesha halmashauri mapato inayostahili.
“Halmashauri yetu ili iongeze mapato ya ndani inategemea mazao kama korosho na ufuta, hivyo, kama sisi tutakuwa tunasinzia au tunakosa usimamizi mzuri na kusababisha korosho kutoroshwa, mapato yatapotea, sitamvumilia mtumishi yeyote atakayekuwa miongoni mwa wanaotorosha korosho,” alieleza Kimara.
Kimara alifafanua atazungumza na Mkuu wa Wilaya ya Kibiti ili kuimarisha usimamizi na doria za kudhibiti utoroshaji wa korosho, akieleza kuwa yuko tayari kushiriki doria hizo usiku na mchana inapohitajika.
Kadhalika, amesisitiza umuhimu wa kuhakikisha wakulima wanapata haki zao kwa wakati ili kupunguza malalamiko na kuimarisha imani yao katika mfumo wa biashara ya korosho.
Amewataka wakulima kutumia vizuri mapato wanayopata kutokana na mauzo ya mazao yao kwa kuyapa kipaumbele mahitaji ya msingi na shughuli za maendeleo ya kiuchumi.
Related Stories
RAIS SAMIA ATEUA MABOSI WAPYA TTB NA TBA
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, amefanya uteuzi wa viongozi wawili wa taasisi za Serikali, akiwemo Mkurugenzi Mkuu wa…