Ndejembi: Mradi wa TAZA ni chachu ya maendeleo
Na mwandishi wetu, Gazetini
MAKAMU wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Deogratius Ndejembi, amesema Mradi wa Kuunganisha Gridi za Umeme za Tanzania na Zambia (Tanzania–Zambia Interconnector Project – TAZA) ni uwekezaji muhimu utakaokuwa chachu ya maendeleo ya kiuchumi katika mikoa ya Nyanda za Juu Kusini kwa kuimarisha upatikanaji wa umeme wa uhakika, kuongeza uzalishaji na kufungua fursa mpya za uwekezaji.
Ndejembi ameyasema hayo leo, Alhamisi, Oktoba 15, 2026, wakati wa ziara ya kukagua maendeleo ya utekelezaji wa Mradi wa TAZA, ikiwemo miundombinu ya vituo vya kupokea na kupoza umeme vya Malangali mkoani Rukwa na Nkangamo mkoani Songwe.
Akizungumza katika Kituo cha Kupokea na Kupoza Umeme cha Malangali, Ndejembi amesema Mkoa wa Rukwa umekuwa ukikabiliwa na changamoto ya upatikanaji wa umeme wa kutosha, hali inayoathiri shughuli za uzalishaji na ukuaji wa uchumi wa mkoa huo.
Ameeleza kuwa kwa sasa Mkoa wa Rukwa hupokea takribani megawati 16 za umeme, wakati mahitaji yake yakifikia megawati 30. Upungufu huo huathiri shughuli mbalimbali za kiuchumi, hususan uchakataji wa mazao ya kilimo, na kuwafanya baadhi ya wakulima kuuza mazao ghafi badala ya kuyasindika ili kuongeza thamani na kipato chao.
“Kwa maelekezo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Samia Suluhu Hassan, ilielekezwa kuwa Mkoa wa Rukwa uunganishwe na Gridi ya Taifa ili kukabiliana na changamoto ya upatikanaji wa umeme. Ndiyo maana mradi huu ulianza kutekelezwa mwaka 2023,” amesema Ndejembi.
Amesisitiza kuwa umeme wa uhakika ni msingi muhimu wa maendeleo, kwani utawezesha wananchi kupanua shughuli za biashara, kuanzisha viwanda, kuongeza thamani ya mazao ya kilimo na kuvutia wawekezaji, hatua zitakazochochea ajira na kuboresha maisha ya wananchi.
Mradi wa TAZA unahusisha ujenzi wa njia ya kusafirisha umeme wa msongo wa kilovoti 400 yenye urefu wa takribani kilometa 618 kutoka Iringa hadi Malangali mkoani Rukwa.
Akiwa katika Kituo cha Kupokea na Kupoza Umeme cha Nkangamo mkoani Songwe, ambacho ujenzi wake umefikia asilimia 83, Mhe. Ndejembi amesema mradi huo utasaidia kuondoa changamoto za muda mrefu za upatikanaji wa umeme na kuimarisha uwezo wa miundombinu ya nishati kukidhi mahitaji yanayoongezeka.
“Laini hii ina urefu wa kilometa 618 kutoka Iringa hadi Rukwa na inakwenda kuondoa kero ya muda mrefu ya changamoto ya umeme, huku ikifungua fursa zaidi za maendeleo ya kiuchumi,” amesema Ndejembi.
Aidha, amesema nafasi ya Tanzania kijiografia inaipa fursa ya kuwa kiunganishi muhimu katika biashara ya umeme kati ya nchi za Afrika Mashariki na Kusini mwa Afrika. Kupitia Mradi wa TAZA, Tanzania itaimarisha uwezo wake wa kushirikiana na nchi jirani, ikiwemo Zambia, katika biashara ya nishati kupitia Mfumo wa Ushirikiano wa Umeme Kusini mwa Afrika (Southern African Power Pool – SAPP).
Ndejembi amewataka wananchi kulinda miundombinu ya umeme inayojengwa kwa gharama kubwa za Serikali, akieleza kuwa miundombinu hiyo ni mali ya umma inayolenga kuboresha huduma za nishati, kukuza uchumi na kuleta maendeleo endelevu.
Utekelezaji wa Mradi wa TAZA ni sehemu ya jitihada za Serikali za kuimarisha Gridi ya Taifa, kupanua upatikanaji wa umeme wa uhakika na kutumia nishati kama kichocheo cha maendeleo ya viwanda, biashara, kilimo na uwekezaji nchini. Ndejembi amewataka wananchi kulinda miundombinu ya umeme inayojengwa kwa gharama kubwa za Serikali, akieleza kuwa miundombinu hiyo ni mali ya umma inayolenga kuboresha huduma za nishati, kukuza uchumi na kuleta maendeleo endelevu.
Utekelezaji wa Mradi wa TAZA ni sehemu ya jitihada za Serikali za kuimarisha Gridi ya Taifa, kupanua upatikanaji wa umeme wa uhakika na kutumia nishati kama kichocheo cha maendeleo ya viwanda, biashara, kilimo na uwekezaji nchini.
The post Ndejembi: Mradi wa TAZA ni chachu ya maendeleo appeared first on gazetini .
The full article is being collected. Available text is shown for now.