UDSM YAIMARISHA USHIRIKIANO WA KIMKAKATI NA UBORA WA TAALUMA

NA EMMANUEL MBATILO, DAR ES SALAAM
CHUO Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) kimesisitiza umuhimu wa kuimarisha ubora wa kitaaluma, utafiti wenye tija, utawala bora na ushirikiano wa kimkakati na wadau wa maendeleo ili kuchangia ukuaji wa uchumi na maendeleo ya Taifa.
Wito huo umetolewa na Mwenyekiti wa Baraza la Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Balozi Mwanaidi Sinare Maajar, na Makamu Mkuu wa Chuo hicho, wakati wa Mahafali ya 56 ya UDSM yaliyofanyika Oktoba 15, 2026.
Akizungumza katika mahafali hayo, Balozi Maajar amesema ushirikiano wa kimkakati katika sekta muhimu za uchumi unapaswa kuleta manufaa kwa Chuo, Serikali, sekta binafsi na jamii, huku ukilinda hadhi ya taasisi na kuendana na maslahi ya muda mrefu ya Chuo na Taifa.
Amesema ubora wa kitaaluma unabaki kuwa msingi wa hadhi ya UDSM, akisisitiza kuwa wahitimu wanapaswa kuwa na uwezo wa kufikiri kwa kina, kutumia teknolojia, kubuni na kutatua changamoto zinazoikabili jamii.
Ameongeza kuwa tafiti zinazofanyika chuoni hapo zinapaswa kuleta matokeo yanayoonekana katika maisha ya wananchi, kusaidia maamuzi ya Serikali na sekta binafsi, pamoja na kuboresha sera, huduma na uzalishaji.
Balozi Maajar, amesema Baraza litaendelea kusimamia ubora wa kitaaluma, maadili, tija ya utafiti na uhusiano wa karibu kati ya Chuo na jamii, huku likihakikisha kuwa maamuzi, uwekezaji na matumizi ya mali za taasisi yanazingatia uwazi, uwajibikaji na utawala bora.
Akizungumza na wahitimu, amewataka kutumia elimu waliyoipata kulitumikia Taifa kwa uadilifu na weledi, akisisitiza kuwa shahada wanazopokea ni dhamana ya kuwajibika kwa jamii na kulinda heshima ya Chuo walikotoka.
Kwa upande wake, Makamu Mkuu wa Chuo hicho, Profesa Anangisye amesema UDSM imepanua ushirikiano na wadau wa ndani na nje ya nchi katika kuimarisha mafunzo, utafiti na ubunifu unaochochea maendeleo ya Taifa.
Amesema Chuo kimeingia makubaliano ya miaka 10 na Barrick Tanzania, ambayo utekelezaji wake umeanza kupitia mafunzo, utafiti, ufadhili wa masomo, mafunzo kwa vitendo na uhawilishaji wa teknolojia katika sekta ya madini.
Aidha, amesema UDSM imezindua Karakana ya Kubadilisha Magari Kutumia Gesi Asilia iliyogharimu Sh bilioni 1.52, itakayoendeshwa na Chuo hicho kupitia ushirikiano wa kimkakati na Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC).
Ameeleza kuwa mradi huo ni sehemu ya mchango wa UDSM katika kukuza matumizi ya nishati safi, kutumia rasilimali za ndani na kuunga mkono malengo ya maendeleo ya Taifa.
Vilevile, amesema Chuo kimeingia ushirikiano wa miaka mitano na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) pamoja na Taasisi ya Sayansi na Teknolojia ya Nelson Mandela (NM-AIST) kwa ajili ya kuimarisha matumizi ya Akili Mnemba, uchambuzi wa takwimu na ubunifu unaotegemea ushahidi.
Profesa Anangisye amewataka wahitimu kutokata tamaa endapo watachelewa kupata ajira serikalini au katika sekta binafsi, akiwashauri kutumia elimu waliyoipata kubuni fursa katika ujasiriamali, kilimo-biashara, uchumi wa kidijitali, utafiti na huduma za kitaalamu.
Amesema ajira haipaswi kuonekana kuwa ni kufanya kazi ofisini pekee, bali wahitimu wanapaswa kutumia maarifa yao kutatua changamoto za jamii na kuanzisha fursa zitakazochangia maendeleo yao binafsi na Taifa kwa ujumla.
The full article is being collected. Available text is shown for now.